Monday, December 21, 2009

NATOA LAKINI SIPOKEI – NIFANYEJE?







Kuna wakati fulani, mtu mmoja alinifuata baada ya kipindi nilichokuwa nafundisha Neno la Mungu juu ya utoaji, na akaniuliza hivi; “Kwa nini mimi nimekuwa natoa zaka na sadaka nyingi lakini sipokei? Hata miradi niliyo nayo haifanikiwi nilivyokusudia – ni kwa nini iwe hivyo.






Inawezekana na wewe unayesoma ujumbe huu sasa una maswali kama haya. Hayo ni maswali ya msingi na ni muhimu tupate ufumbuzi wake. Hata mkulima ambaye alipanda mbegu katika shamba, na asipate kitu au apate mavuno machache, atajiuliza maswali kumetokea kitu gani.






Tukumbuke ya kuwa si mapenzi ya Mungu tuwe maskini – tuwe na hali ngumu kimavazi, chakula na kiafya. Pia, tukumbuke ya kuwa ni tabia ya kiuungu mtu kutoa na kutegemea kupokea. Ingawa si lazima upate toka kwa mtu huyo huyo uliyempa, - maana Mungu anaweza kumgusa mtu mwingine akupe – lakini utaratibu wa Mungu unabaki pale pale, ukitoa tegemea kupokea.






Ni kitu gani kinasababisha mtu asipokee na huku amekuwa akijitahidi kutoa? Biblia inatuambia ya kuwa tukiwa waaminifu katika utoaji, Mungu atatumwagia baraka, “hata isiwepo nafasi ya kutosha ya kuziweka” – Je! umewahi kumsikia mkristo yo yote akisema amepata baraka nyingi mno hata amekosa mahali pa kuziweka?






Sababu zifuatazo zitatusaidia kujua ni kwa nini hatufanikiwi katika utoaji wetu – na hata hatupokei kama tulivyotegemea na kutarajia;






1. KUVUNJA MIIKO AU UTARATIBU WA UTOAJI






Kila jambo lina utaratibu wake – usipoufuata usitegemee mavuno mazuri. Kilimo cha mahindi kina utaratibu wake wa upandaji na palizi tofauti na kilimo cha ngano au cha kabichi. Ndiyo maana wataalamu wa kilimo, walianzisha kampeni za kuwafundisha wakulima juu ya “kilimo cha kisasa” ili kiwasaidie wakulima kupata “mavuno” zaidi toka katika mashamba yao.






Hata katika “kupanda na kuvuna” au “kutoa na kupokea” katika mambo ya Mungu kuna utaratibu wake. Ukienda kinyume na utaratibu huo, usitegemee mavuno ya kuridhisha toka katika utoaji wako






Kwa mfano hebu soma na kutafakari maneno haya yafuatayo:






“Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama ilivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu” (2Wakorintho 9:6,7).


“….wala si kama kitu kitolewacho kwa unyimivu” (2Wakorintho 9:5).






Utaona katika mistari hiyo Mungu ametueleza kwa kiasi fulani utaratibu ambao anataka ufuatwe mtu akitaka kuvuna katika utoaji wake. Je! unafuata utaratibu huu katika utoaji wako?






Utaratibu huo ni huu; utoaji wako uwe si haba (au kidogo) bali uwe kwa ukarimu. Ukitoa kidogo utapata kidogo – bali ukitoa vingi utapata vingi. Ndiyo maana imeandikwa;






“Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. KWA KUWA KIPIMO KILE KILE MPIMACHO NDICHO MTAKACHOPIMIWA” (Luka 6:38)






Kama unataka kutoa sadaka tu “ kama ulivyokusudia moyoni mwako”. Kama ulikusudia kutoa shilingi 100/= toa shilingi 100/=. Fanya hivi siku zote na utafanikiwa.






Tena, utoaji unatakiwa ufanyike “si kwa huzuni; wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu “… na wala si kwa unyimivu”.






Michango mingi iliyomo makanisani siku hizi wakati mwingine inafanyika kwa kulazimishana. Mtu anatakiwa atoe kwa kupenda kwake toka moyoni mwake – SI KWA LAZIMA. Kumlazimisha mtu kutoa ni kwenda kinyume cha utaratibu wa utoaji.






Wakristo wengi wamekosa baraka au mafanikio katika utoaji kwa sababu wanatoa huku WANAHUZUNIKA AU WANALALAMIKA! Wengi wanawanung’unikia viongozi wa makanisa yao kuwa wanatumia fedha au vitu vibaya. Kama una wasiwasi na matumizi ya matoleo yako – yaombee kwa Mungu ayalinde yatumike kwa utukufu wake kuliko kulalamika.






Wengine wanahuzunika na kulalamika kuwa michango imezidi. Je! umewahi kumsikia mkulima akihuzunika au kulalamika kwa kuwa ameongezewa shamba la kulima na kupanda? Hakuna. Mkulima halalamiki bali anafurahi kwa kuwa amepata eneo kubwa zaidi la kupanda umeongezewa eneo la KUPANDA ili AVUNE ZAIDI. Ni eneo la kukusaidia kutoa zaidi ili UPOKEE ZAIDI!






2. IBILISI AMEZUIA BARAKA ZAKO;






Kati ya baraka ambazo zinapatikana kutokana na mtu kuwa mwaminifu katika utoaji wa zaka (fungu la kumi) na dhabihu (matoleo mbalimbali) na kuzidiwa wakati wa matatizo, Mungu alisema hivi;






“Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba ….” (Malaki 3:11).






Ni wazi kuwa aliye nyuma ya kuharibika kwa mazao shambani au biashara ni yule ‘alaye’ ambaye ni Ibilisi. (Hii ni kama mkulima au mfanya biashara amefanya anachotakiwa kukifanya kilicho ndani ya uwezo wake).






Kinyume cha jambo hili ni kwamba usipokuwa mwaminifu kutoa fungu la kumi toka katika mazao ya shamba lako, usitegemee Mungu akupiganie wakati mharibu anapoingilia mimea yako na kuiharibu. Vile vile usipokuwa mwaminifu kutoa fungu la kumi toka katika mapato ya biashara yako, usitegemee Mungu akusaidie wakati mharibu anapoingilia biashara yako na kuiharibu.






Inawezekana unatoa sadaka, na huoni baraka zozote zinazotokana na kutoa kwako – hebu angalia na jichunguze kama umekuwa mwaminifu katika kutoa ZAKA KAMILI. Kwa mfano kama fungu la kumi la pato lako ni shilingi 2,000 – toa zaka kamili yaani shilingi 200/=. Usitoe pungufu ya hiyo maana haitakuwa zaka KAMILI.






Ikiwa umekuwa mwaminifu katika kutoa Zaka kamili na dhabihu halafu huoni matokeo yake basi, tumia mamlaka ya Jina la Yesu Kristo – mfunge na kumkemea ibilisi ambaye ndiye mharibu wa mali yako aondoe mikono yake juu ya mali yako.






Kumbuka Yesu Kristo alisema;


“Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalofunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni” (Mathayo 16:19).






Kuna mtumishi mmoja wa Mungu ambaye anasimulia jinsi ambavyo mkulima mmoja wa pamba alivyosaidika na uwezo wa jina la Yesu Kristo.






Huyo Mkulima alikuwa mwaminifu katika kumtolea Mungu fungu la kumi la mapato ya shamba lake kila mwaka, na alikuwa haelewi kwa nini pamba yake ilikuwa haifunguki ingawa muda wa kufunguka na kuchanua ulikuwa umefika. Wataalamu wa kilimo cha pamba walikuja kuliangalia shamba hilo lakini hawakuweza kumsaidia mkulima huyo kutatua tatizo hilo.






Mtumishi wa Mungu huyo alifika hapo, na alisikia habari ya mahangaiko ya mkulima huyo. Baada ya kufahamu ya kuwa mkulima huyo alikuwa mwaminifu katika kutoa fungu la kumi – alimwambia waende shambani ili waombe.






Huyo mtumishi wa Mungu wakiwa shambani na mkulima huyo; - akimkumbusha Mungu juu ya ahadi yake ya Malaki 3:7-11. Na mwishoni akamwamuru ibilisi aondoke kwenye pamba hiyo. Mara tu baada ya kumaliza sala hiyo – pamba ilianza kufunguka na kuchanua! Bwana asifiwe sana kwa uwezo huu ulivyo wa ajabu.






Usibaki unalalamika na kuhangaika kama vile mtu asiyejua ahadi za Mungu. Simamia haki zako ndani ya Kristo kwa kuwa mtendaji wa neno na utafanikiwa.






3. KUTOKUPANDA KATIKA UDONGO MZURI






Utoaji ni sawasawa na upandaji. Mtu akipanda anategemea kuvuna pia. Kwa hiyo mtu akitoa anategemea kupokea.






Mkulima yo yote akitaka mavuno mazuri toka shambani mwake kati ya vitu anavyoviangalia ni aina ya mbegu na aina ya udongo. Siku zote atapanda kwenye udongo mzuri wenye rutuba.


Mfanya biashara siku zote anataka aweke mtaji wake katika vitu vitakavyomletea faida kibiashara na siyo hasara.


Lakini, inasikitisha kuona kuwa inapofika wakati wa utoaji – wakristo wanatoa tu bila kuangalia kwanza “udongo mzuri” ni upi ili utoaji wao uwaletee matokeo mazuri.






Biblia inatuambia katika mfano wa mpanzi ya kuwa mbegu zingine“…. Zikaanguka penye udongo ulio mzuri, zikazaa matunda, zikimea na kukua, na kuzaa, moja thelathini, moja sitini, na moja mia” (Mathayo 4:8).






Je, “udongo mzuri” unaoleta faida nzuri ni upi? Sehemu za kutoa zenye matokeo au mavuno mazuri ni hizi zifuatazo;






(a) Katika nyumba ya Mungu – kanisani ili kuendeleza kazi ya Mungu – soma Malaki 3:10-11; na Kumbukumbu ya Torati 8:18.






(b) Kuwasaidia watumishi wa Mungu na watakatifu wake kwa vitu/mali ulizo nazo. Soma 1Wafalme 17:10-24 na 2Wakorintho 9:10-13.






(c) Kuwasaidia maskini kwa vitu/mali ulizo nazo. Soma 2Wakorintho 9:8-9.






Angalia upandaji wako katika utoaji – je! umepanda kwenye udongo ulio mzuri?






4. KUKATA TAMAA






Wagalatia 6:9 inasema hivi; “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho”.


Tafsiri iliyo nyepesi inasema, “maana tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa”.


Wakristo wengi wanatoa lakini hawana uvumilivu. Mkulima asipokuwa mvumilivu kusubiri mazao ya shamba lake yanayokuja kwa wakati wake – hawezi kuvuna alichopanda.


Vile vile mtoaji asiyejifunza kumvumilia Mungu ili amletee matokeo ya utoaji huo kwa WAKATI WAKE – hawezi kuvuna alichopanda.


Mungu si mwongo! Wala ahadi zake hazijui kusema uongo. Alichoahidi atatenda. Ukitoa utapokea KWA WAKATI WAKE USIPOKATA TAMAA.


Usianze kutafuta njia za mkato ili ufanikiwe – uwe mvumilivu ulichopanda kwenye udongo mzuri utavuna.


Mkumbuke Ibrahimu alivyovumilia. Biblia inasema hivi;


“Lakini akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutokuamini, bali alitiwa nguvu kwa imani, akimtukuza Mungu; huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi” (Warumi 4:20-21).






5.KUTOA KWA MAJIVUNO NA KUTAFUTA KUSIFIWA NA WATU






“Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni. Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili WATUKUZWE NA WATU. Amin, nawaambieni,wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume; sadaka yako iwe kwa siri; na BABA YAKO AONAYE SIRINI ATAKUJAZI” (Mathayo 6:1- 4)


No comments:

Post a Comment